Nikikutajia jina Emmanuel mkono unaweza usigundue kwamba namuongelea nani lakini nikikutajia nyimbo kama Tanzania ya Roma Mkatoliki, Niaje Nivipi ya Joh Makini na Nikki wa pili, Rizione ya Izo Bizness, Gere ya Weusi au Mfalme ya Mwana Fa na G Nako utagundua kwamba nyimbo zote hizi zinafanana katika jambo moja, zote zimewahi kuwa hit songs hapa nchini na zote zilitengenezwa na mtayarishaji mmoja Nahreel aka Emmanuel mkono.
Wazungu wao wana msemo kwamba “from small acorns mighty oaks grow” na hiki ndicho kilichotokea katika safari ya Nahreel. Baba yake mzazi alipanda mbegu ndogo tuu kupitia kinanda alichomnunulia Nahreel Pamoja na mwalimu wa kumfundisha. Mzee Mkono alitamani Nahreel akapige kinanda kanisani lakini Mungu alikuwa na mpango mwingine juu ya nyota hii ambayo ilikuja kung’aa sana miaka kadhaa baadae.
Wengi tumezoea kusikia hadithi za Watoto waliozaliwa na vipaji na kutimiza ndoto zao kupitia vipaji hivyo. Kwa Nahreel ilikua tofauti kidogo Pamoja na kwamba alibarikiwa mikono ya dhahabu na masikio ya kipekee bado alihitaji kujituma na kujiongeza sana ili aweze kuwa katika ubora ambao leo sisi tunaufahamu. YouTube ndio mahali alipojifunza mambo mengi kuhusu production na kupitia kujituma kwake akaweza kutengeneza hit baada ya hit. Ndoto yake ilikua kuwa na nyimbo hata kumi katika chat za muzki za Tanzania.
Pamoja na kwamba Nahreel alitaka kuwa mtayarishaji wa muziki na ukweli kwamba baba yake ndiye aliyempa kinanda lakini bado hakuamini sana katika muziki na ndio maana ilimbidi nahreel awaage pale Kama Kawa Records aende kwanza India kusoma kama ambavyo baba yake alihitaji. Akiwa India alipokua anasoma shahada yake ya kwanza ya Computer Science hakuacha kugonga beats kali, hakuacha kuendelea kuipalilia ndoto yake. Akamaliza shule na kurudi nyumbani kuendeleza marathon yake ya muziki wakati huu akiwa pale Home Town Records. Ni pale Home Town Records ndipo ilipozaliwa Navy Kenzo moja kati ya makundi bora ya muziki hapa nchini.
Nahreel anabaki kuwa moja kati ya watayarishaji bora kabisa wa muziki kuwahi kutokea hapa nchini na kinachomuongezea ubora huo ni ukweli kwamba yeye ni muimbaji pia. Tumepata nafasi ya kuyaona na kuyafaidi matunda ya mbegu ndogo aliyoipanda mzee Mkono wakati nahreel akiwa na miaka 14 tuu. Bado tunaendelea kuyafaidi matunda ya mti huu mkubwa ambao ni zawadi kwa kizazi chetu.